Msanii wa muziki kutoka Kenya Willy Paul ameachia wimbo mpya wa gospel unaoitwa “Mkono Wako,” hatua inayotafsiriwa na wengi kama kurejea kwake rasmi katika muziki wa injili.
Willy Paul, ambaye awali alijipatia umaarufu kupitia nyimbo za gospel kabla ya kuhamia muziki wa kidunia, ametoa wimbo huo akiwa na ujumbe wa kiroho unaozungumzia kumtegemea Mungu katika maisha.
Katika wimbo “Mkono Wako,” Willy Paul anaeleza safari yake ya maisha na changamoto alizopitia, akisema aliwahi kujikuta akipotea lakini akarejea kwa Mungu.
Tofauti na midundo ya kasi aliyokuwa akitumia kwenye baadhi ya nyimbo zake za hivi karibuni, wimbo huo mpya una mpangilio wa ala tulivu unaochanganya ladha ya Zouk na Afrobeat, huku ukibeba ujumbe mzito wa kiroho.
Hata hivyo wimbo wa Mkono Wako, unatajwa kuwa na msukumo kutoka kwa hit single yake “Sitolia,” aliowahi kuimba pamoja na Gloria Muliro, uliompa umaarufu mkubwa katika tasnia ya muziki wa injili miaka iliyopita.