
Msanii wa Kenya VJ Patelo ameibuka na lawama nzito dhidi ya msanii Willy Paul kwa madai ya kutomlipa baada ya kumshirikisha kwenye video yake mpya ya muziki. Inadaiwa kuwa kabla ya kurekodi, Willy Paul alimuahidi Patelo mafuta ya gari pamoja na kifuta jasho, lakini baada ya kufika kwenye video shoot akiwa na mkewe Diana, msanii huyo alianza kumpuuza na kutojibu simu zake.
Patelo amesema vitendo vya aina hiyo vinachangia kudidimiza muziki wa Kenya na kupelekea mashabiki wengi kugeukia muziki wa Tanzania. Kulingana naye, wasanii wa Tanzania wanashinda kwenye chati za muziki nchini Kenya kwa sababu ya nidhamu na uwajibikaji, jambo ambalo wasanii wa Kenya bado wanakosa kuzingatia.
Ameonya kuwa hana muda wa kushirikiana na wasanii wasioweza kumlipa ipasavyo na amesisitiza kwamba kazi yake ina thamani inayopaswa kulipwa kwa heshima. Aidha, amewataka wasanii wenzake kuacha tabia ya kutothamini washiriki wanaowaunga mkono katika kazi zao.
Mpaka sasa, Willy Paul hajajibu hadharani madai yaliyotolewa dhidi yake, na mjadala kuhusu suala hili unaendelea kushika kasi miongoni mwa mashabiki wa muziki.