Gossip

Kataleya na Kandle Wapanga Kuzaa Watoto Wakati Mmoja

Kataleya na Kandle Wapanga Kuzaa Watoto Wakati Mmoja

Wasanii wawili maarufu kutoka Uganda, Kataleya na Kandle, wameweka wazi mpango wao wa kupata ujauzito kwa wakati mmoja, hatua ambayo imezua hisia mseto miongoni mwa mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na kituo cha redio cha Galaxy FM, wawili hao, ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu tangu walipoingia kwenye tasnia ya muziki, wameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wao wa karibu na kuonyesha mshikamano wa kipekee katika maisha ya kibinafsi, sawa na walivyofanya katika kazi zao za muziki.

“Tuna ndoto ya kuwa mama kwa wakati mmoja. Tumejipanga na tunajua kile tunachokitaka. Tunaamini tunaweza kulea watoto wetu kama marafiki vile sisi tulivyokua,” alisema Kataleya huku Kandle akiongeza, “Huu si mpango wa kiki, ni uamuzi wa kweli ambao tumeufanya kwa upendo na makubaliano ya kina.”

Ingawa hawakutoa maelezo ya kina kuhusu lini mpango huo utaanza kutekelezwa au kuhusu wenza wao, walisisitiza kuwa wamefikia uamuzi huo kwa pamoja baada ya mazungumzo ya kina kuhusu maisha yao ya baadaye.

Taarifa hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki. Baadhi wameipongeza kama hatua ya kuonyesha mshikamano na uthubutu wa wanawake katika kufanya maamuzi ya maisha, huku wengine wakieleza tahadhari juu ya athari za kijamii na kihisia kwa maamuzi ya aina hiyo.