Uongozi wa lebo ya muziki ya WCB Wasafi umejitokeza kukanusha taarifa zinazozagaa mitandaoni zikidai kuwa msanii wao, Zuchu, amekataa kushirikiana na wasanii wa Kenya kwa madai kwamba baadhi ya Wakenya walimtukana Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, WCB imesisitiza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na ni njama za kuzua mtafaruku kati ya mashabiki wa pande mbili. Uongozi huo umesema kuwa Zuchu hana uhusiano wowote na kauli inayodaiwa kunukuliwa kwenye moja ya blogu nchini Kenya, na kwamba msanii huyo ameendelea kuwa na uhusiano mzuri wa kikazi na mashabiki wake kote Afrika Mashariki.
Taarifa hizo za WCB zimekuja muda mfupi baada ya uvumi huo kushika kasi mtandaoni, hasa baada ya kufufuliwa kwa nakala ya blogu iliyodai kuwa Zuchu alinukuliwa akisema hatafanya kazi na wasanii kutoka Kenya.
Zuchu kwa sasa yupo nchini Kenya ambapo anatarajiwa kutumbuiza kesho kwenye fainali za CHAN zitakazofanyika kesho kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani. Atashiriki jukwaa moja na Savara wa Sauti Sol kutoka Kenya pamoja na Eddy Kenzo wa Uganda.