Msanii aligeukia biashara nchini Kenya, KRG The Don, ametangaza rasmi kwamba atawania nafasi ya Useneta wa Kaunti ya Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii, KRG amesema kuwa huu ni wakati wa viongozi wapya na vijana kuingia katika uongozi ili kuleta mabadiliko ya kweli jijini Nairobi.
Katika ujumbe wake, KRG The Don ametoa wito mkali kwa Wakeny hasa vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kama wapiga kura, akisema kuwa bila kuwa na kadi ya mpiga kura, sauti yao haiwezi kusikika kwenye maamuzi makubwa ya nchi.
Amesema kuwa vijana wa Nairobi wana changamoto nyingi zinazohitaji mtu mwenye mtazamo mpya, ubunifu na uthubutu kuzitatua. Amependekeza ajenda kama ukuaji wa biashara ndogo, usalama, na fursa kwa vijana kuwa miongoni mwa malengo yake endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo.
Tangazo hilo limepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni. Baadhi ya mashabiki na wafuasi wake wameonyesha kumkubali na kumtia moyo kuingia kwenye siasa, wakisema kuwa ushawishi wake mkubwa unaweza kuleta mabadiliko chanya. Wengine, hata hivyo, wamesema wanataka kuona sera na mipango yake kwa kina kabla ya kufanya uamuzi