
Rapa mkongwe kutoka Marekani 50 Cent amedai kwamba bado waliokuwa wasanii wa kundi la G-Unit wanamtupia lawama kwa kushindwa kwao kufanikiwa katika muziki.
Kwenye mahojiano yake na 97.9 The Box, 50 Cent ambaye alikuwa kichwa cha kundi hilo (Label) amezungumza na kusema siku zote watu au wasanii humtupia lawama kiongozi na sio taasisi au kampuni waliopo.
“Kuna ambao huwa wananiomba radhi kwa maneno yao. Lakini unajua kidonda kipo sehemu moja, unapokuwa kwenye nafasi ya kuendesha gari, kiti cha dereva, mara nyingi pale mambo yakiwa hayaendi sawa sio kosa lako. Ukiwauliza wasanii kwanini walishindwa kufanikiwa, siku zote wataitupia lawama Record Label” alisema 50 Cent na kuendelea
“Hivyo mimi binafsi nilipata kuwa Record Label, hivyo wasanii wote ambao walikuwepo na mambo yao hayakwenda vile walivyotarajia, ni makosa yangu kwamba sikufanikisha mambo yao. Wananitupia lawama Mimi binafsi na sio kampuni tena.” alimaliza 50 Cent.
Chini ya uongozi wa 50 Cent, Kundi la G-Unit lilikuwa na wasanii kama Lloyd Banks, Young Buck, Tony Yayo, The Game na DJ Whoo Kid.