
Mwanamuziki, Kidis, anayefahamika kwa nyimbo zake maarufu zilizochangia pakubwa kukuza muziki wa Kenya, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu hali yake ya kifedha na mikakati anayotumia kuhakikisha anajimudu kimaisha nje ya tasnia ya muziki.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, Kidis alieleza kuwa kwa sasa ana utajiri unaokadiriwa kuwa shilingi 700,000. Hata hivyo, alikiri kuwa kiwango hicho hakijatokana na muziki pekee, bali kupitia juhudi binafsi katika biashara ndogo ndogo.
“Usanii ni mzuri na wa kujivunia, lakini huwezi kutegemea muziki pekee kupata kipato cha maana kila wakati. Nimeamua kujihusisha na biashara kama kuuza bedsheets na makaa ili kuongeza kipato na kujenga maisha ya kudumu,” alisema.
Kidis alitoa wito kwa wasanii wenzake na vijana kwa ujumla kutafuta mbinu mbadala za kujiongezea kipato, akisisitiza kuwa hali ya sasa ya uchumi na ushindani mkubwa katika tasnia ya burudani imefanya mapato kutoka kwa muziki kutokuwa ya kutegemewa kwa asilimia mia moja.
Kwa maoni ya wengi, hatua ya Kidis ya kuzungumza kwa uwazi kuhusu hali ya kifedha na jitihada zake nje ya muziki ni kielelezo cha ujasiri na msukumo kwa wasanii wengine wanaotafuta mafanikio ya kweli. Amejidhihirisha kuwa si tu msanii wa vipaji bali pia mjasiriamali mwenye maono, anayefahamu umuhimu wa kuwa na vyanzo vya mapato mbadala.