
Msanii nyota wa Afrobeats kutoka Nigeria, Davido, amewashangaza mashabiki wake kwa kufichua kwamba angekuwa mwandishi wa habari kama hangejikita kwenye muziki. Kauli hiyo ya kushangaza ilitolewa wakati wa mahojiano ya moja kwa moja kwenye Beat 96.1FM, ambako msanii huyo alizungumza kwa undani kuhusu maisha yake nje ya jukwaa.
Katika mahojiano hayo, Davido alieleza jinsi ambavyo kampeni ya kutangaza albamu yake mpya imekuwa ya kuchosha, lakini kwa upande mwingine, anafurahia sana mazungumzo na mikutano na wanahabari, tofauti na wasanii wengi wa kiwango chake.
“Nimekuwa nikifanya promo kali kwa ajili ya albamu yangu – si kazi rahisi. Sina haja ya kufanya promo lakini napenda. Napenda kuongea. Watu wengi hawajui kwamba mbali na kusomea usimamizi wa biashara, pia nimesomea masoko. Kwa hiyo napenda mazungumzo. Kama ningekuwa na podcast, ningeweza kuzungumza siku tatu au nne mfululizo.”
Tofauti na wasanii wengi wanaoepuka kamera na mahojiano, Davido anaamini kuwa mazungumzo ni sehemu ya sanaa, na kwamba huwa anajihusisha sana na taarifa mbalimbali za kijamii na kisiasa.
“Ni sehemu ya kuwa msanii, kwa mtazamo wangu. Si kila mtu hupenda kuzungumza, lakini mimi napenda. Nikikutana na mtu, napenda kuongea. Napenda habari. Ukiingia nyumbani kwangu, kila mara mimi huhakikisha kuna taarifa – huwezi kukosa CNN kwenye runinga ya sebuleni.”
Akiendelea kufunguka, Davido alieleza kuwa mara nyingi akiwa nyumbani hujikuta akifanya utafiti kuhusu mambo mbalimbali, ishara kuwa ana kiu ya maarifa na kujua yanayoendelea duniani. Kwa msingi wa mapenzi yake makubwa kwa mawasiliano, Davido alisema kwamba kama hangekuwa msanii, basi angekuwa mtangazaji au mwanahabari.
“Mimi ni mtu ninayependa taarifa. Naona kama nisingekuwa kikamilifu kwenye muziki, basi ningekuwa kwenye kitu kama uandishi wa habari. Napenda kuwaeleza watu kile ninachofanya.”
Aidha, alizungumzia kuhusu umaarufu wake mitandaoni, akisema kuwa sababu mojawapo ni kujishughulisha, kushiriki, na kuwasiliana moja kwa moja na mashabiki wake.
“Watu huuliza kwa nini nina followers wengi – ni kwa sababu najihusisha na watu, na ninafanya kazi kila wakati.”
Kwa kauli zake, Davido anaonesha kuwa yeye si msanii wa kawaida tu, bali ni msomi wa mawasiliano, mpenzi wa taarifa, na mtu anayeamini kuwa muziki na mawasiliano vinaenda pamoja. Hali hii huenda ikamfungulia milango ya vipindi vya podcast au mahojiano ya runinga siku za usoni.