
Mwanamuziki wa Uganda, Azawi , amefunguka kuhusu uwekezaji mkubwa alioufanya kuboresha tabasamu lake, baada ya kupata mafanikio makubwa chini ya lebo ya Swangz Avenue.
Akizungumza katika mahojiano na mtangazaji wa YouTube, Kasuku, Azawi alieleza kuwa alitumia kiasi cha shilingi milioni 24 za Uganda (UGX) kurekebisha tatizo la meno lililosababishwa na ajali aliyopata alipokuwa katika umri mdogo. Msanii huyo alisema alianguka na kuvunjika taya, hali iliyosababisha mapengo yaliyoathiri muonekano wake kwa muda mrefu.
“Sikuwa na uwezo wa kuyarekebisha zamani, lakini baada ya kupata mafanikio kupitia muziki wangu chini ya Swangz Avenue, niliamua kuweka hilo suala sawa. Ilikuwa ni hatua ya binafsi na ya muhimu kwangu,” alisema Azawi.
Katika mahojiano hayo, Azawi pia aligusia maisha yake ya kimapenzi, akifichua kuwa awali alikuwa katika mahusiano ya muda mfupi, lakini sasa yuko tayari kutulia. Kwa utani, alieleza kuwa hupendelea wanaume warefu na wanene, akisema haavutiiwi na wanaume wenye misuli (six-packs).
Azawi anaendelea kung’ara katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki, na sasa si tu kwa sauti yake ya kipekee, bali pia kwa tabasamu linaloendana na jina lake kubwa.
Swangz Avenue ilimsaini Azawi mwaka 2019 na kumtambulisha rasmi kwa umma tarehe 31 Oktoba mwaka huo. Tangu wakati huo, amejizolea umaarufu kwa nyimbo kama ‘Lo Fit’, ‘Masavu’, ‘Party Mood’, ‘Majje’, ‘Quinamino’, na ‘Ku Sure’.