
Mechi za kuwania ubingwa wa ligi kuu ya mpira wa mikono nchini zinatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwenye uwanja wa Nyayo, huku kivumbi kikitarajiwa kati ya vinara wa ligi ya wanaume NCPB na wapinzani wao wakuu Equity. Timu zote mbili hazijapoteza mechi yoyote msimu huu, na mchezo wao unatarajiwa kuwa wa kuamua bingwa, hasa ikizingatiwa kuwa NCPB wana alama 46 huku Equity wakifuatia kwa alama 44 na mchezo mmoja mkononi.
Katika mechi nyingine za wanaume, Ulinzi, waliopo nafasi ya tatu, watavaana na GSU, huku Strathmore wakikabiliana na Wakanda, wakilenga kumaliza msimu ndani ya tano bora. Ushindani mkali unatarajiwa, hasa kwa timu zinazotafuta nafasi ya kujihakikishia nafasi nzuri msimu ujao.
Kwa upande wa ligi ya wanawake, Ulinzi Sharks watakutana na Daystar siku ya Jumapili, huku Young Zealots wakimenyana na NYS, na JKUAT wakichuana na Fireworks. Hadi sasa, Nairobi Water wanaongoza ligi hiyo kwa alama 26, wakifuatwa na Ulinzi Sharks na Daystar katika nafasi ya pili na tatu mtawalia.