
Msanii na mtangazaji maarufu Daddie Marto ameibuka na kutoa tamko rasmi kufuatia madai mazito yaliyotolewa na mkewe, Koku Lwanga, yanayomhusisha na usaliti wa ndoa pamoja na vitendo vya ukatili wa kimwili na kihisia.
Katika taarifa aliyotoa kupitia mitandao ya kijamii, Marto alikanusha vikali tuhuma hizo, akieleza kuwa zimejengwa kwa msingi wa taarifa potofu na zenye nia ya kumchafulia jina. Akiwa na msimamo wa wazi, alisisitiza kuwa hastahimili wala kuunga mkono aina yoyote ya ukatili, na kwamba hali inayoonyeshwa kwenye mitandao siyo halisi.
“Ningependa kusema kwa uwazi kabisa: sitetei wala siungi mkono ukatili wa aina yoyote, wa kimwili, kihisia, au kisaikolojia. Aidha, nakataa kwa nguvu zote kuwa mhanga wa tuhuma za uongo na zenye madhara makubwa.”
Marto aliendelea kueleza kuwa simulizi inayosambazwa kwa sasa imepotoshwa na haioneshi ukweli kamili wa hali halisi iliyotokea katika maisha yao ya kifamilia.
“Hadithi inayoendelea kusambaa mtandaoni ni ya upande mmoja na imeondoa muktadha muhimu. Inapotosha na inaleta madhara makubwa, si kwa jina langu tu, bali pia kwa watoto wetu, familia zetu, na jamii tunayoishi.”
Haya yanajiri wakati mashabiki na watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiendelea kufuatilia kwa karibu mvutano huu wa wawili hao ambao kwa muda mrefu walionekana kuwa mfano wa ndoa yenye uthabiti na mshikamano.
Kwa sasa, Koku Lwanga bado hajajibu hadharani kauli ya mumewe, huku wengi wakiomba wawili hao kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya faragha na heshima kwa familia yao.