Entertainment

Arrow Bwoy Atoa Wimbo Mpya Baada ya Kupigwa na Polisi

Arrow Bwoy Atoa Wimbo Mpya Baada ya Kupigwa na Polisi

Msanii maarufu wa muziki wa Dancehall, Arrow Bwoy, ameibua hisia kali mitandaoni baada ya kuachia wimbo mpya wenye ujumbe mzito unaogusa madhila ya ukatili wa polisi, kufuatia tukio la kushangaza alilokumbana nalo katika maandamano ya hivi karibuni jijini Nairobi.

Katika ujumbe wake wa wazi kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, msanii huyo alieleza kuwa alinusurika kujeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa nyahunyo na kukumbwa na gesi ya kutoa machozi wakati wa maandamano ya amani yaliyokuwa yakipinga sera tata za serikali na ukosefu wa uwajibikaji wa vyombo vya usalama. Alieleza kuwa hali hiyo ilimfanya kutambua uzito wa changamoto ambazo wananchi wa kawaida hukumbana nazo kila siku.

“Sikuwahi jua kuwa siku moja nitakuwa mhanga wa ukatili wa polisi. Ninamshukuru Mungu nilirudi jana nyumbani nikiwa hai – wengine hawakurudi. Naamini kuwa tunaweza kuishi kwa amani iwapo sote tutafuata na kuheshimu sheria. Sikiliza wimbo wangu mpya, link ipo kwenye bio. Bado ni #Mapambano ✊🏿❤️🇰🇪.” Arrow Bwoy aliandika Instagram.

Wimbo wake mpya, “Mapambano”, umetumika kama jukwaa la kuonyesha mshikamano na wananchi waliopoteza maisha au kujeruhiwa katika maandamano hayo, huku ukihimiza utulivu, mshikamano na utawala wa sheria kama njia ya kweli ya kusuluhisha tofauti za kijamii na kisiasa.

Maandamano hayo, yaliyoongozwa na vijana katika zaidi ya kaunti 20 nchini Kenya, yameacha majeraha ya kitaifa baada ya taarifa rasmi kuthibitisha vifo vya watu wasiopungua 16 na wengine wengi kujeruhiwa. Tukio hilo limezua mjadala mpana kuhusu haki za kiraia, uhuru wa kujieleza na matumizi ya nguvu kupita kiasi na vikosi vya usalama.

Arrow Bwoy, ambaye ni miongoni mwa wasanii wachache walioshuhudia na kuathirika moja kwa moja na vurugu hizo, sasa anatumia sauti yake ya kisanii kutoa mwito wa mabadiliko, akihimiza jamii kushikamana na kutafuta suluhisho kwa njia ya amani na haki.