
Klabu ya Chelsea imefanya hatua kubwa katika dirisha la usajili kwa kukamilisha usajili wa wachezaji wane wapya wa safu ya ushambuliaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao wa 2025/26.
Wachezaji waliothibitishwa kusajiliwa ni Jamie Gittens kutoka Borussia Dortmund, Willian Estevão kutoka Palmeiras, João Pedro kutoka Brighton & Hove Albion na Liam Delap kutoka Ipswich Town.
Usajili huu umekuja baada ya klabu hiyo kuonyesha udhaifu katika safu ya ushambuliaji msimu uliopita, ambapo Chelsea ilifunga jumla ya mabao 64, idadi ndogo zaidi miongoni mwa timu nne za juu katika Ligi Kuu ya England.
Katika upande wa ulinzi, Chelsea iliruhusu mabao 43, ikiwa ni ya pili kati ya timu nne bora kwa kuruhusu mabao mengi ikiwa nyuma ya Manchester City walioruhusu mabao 44.
Kuingia kwa Gittens na João Pedro kunatazamiwa kuongeza kasi, ubunifu na chachu ya mabao, huku Estevão akiwa moja ya vipaji vya hali ya juu kutoka Brazil, anayekuja kwa matarajio makubwa. Liam Delap, mshambuliaji mwenye nguvu na muono wa bao, anatazamiwa kuwa chaguo mbadala mwenye tija ndani ya kikosi hicho.
Kocha wa Chelsea amesisitiza kuwa maboresho haya ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kujenga kikosi chenye ushindani ndani na nje ya Uingereza, akiahidi kuwa mashabiki watarajie timu yenye njaa ya mafanikio na soka la kuvutia.