
Rapa maarufu kutoka Kenya, Khaligraph Jones, ameibua mjadala mkali mtandaoni baada ya kudai kuwa wasanii wengi walioko chini ya lebo kubwa za muziki wanapitia hali ngumu kifedha licha ya kuonekana wanaishi maisha ya kifahari.
Kupitia mitandao ya kijamii, Khaligraph alifichua kuwa licha ya kupokea ofa nyingi za kusaini mikataba na lebo mbalimbali, aliamua kusalia huru na kusimamia kazi zake mwenyewe. Anaeleza kuwa wasanii wengi wakubwa wapo kwenye madeni makubwa na kwamba uhuru wa kifedha ndio umemwezesha kuendelea vizuri bila presha ya mikopo au masharti magumu ya mikataba.
Rapa huyo anasema kuwa anathamini uhuru wa kifedha kuliko mvuto wa mikataba inayokuja na majina makubwa lakini haina manufaa ya moja kwa moja. Anaeleza kuwa maisha yake ni ya amani kwa sababu anamiliki kile anachonacho na hana mzigo wa madeni unaomkosesha amani.
“Wengi wao mnaowaona ni wakubwa, lakini wako kwa madeni makubwa sana. Wengine wanateseka kimyakimya. Mimi nilikataa hizo deals zote, niko huru, sina deni, na naball kwa amani na mali yangu,” alisema Khaligraph.
Katika ujumbe huo, Khaligraph alionyesha pia matumaini ya kupata mafanikio zaidi na kuboresha maisha yake, akitaja magari ya kifahari kama sehemu ya malengo yake ya baadaye.
Kauli zake zimezua mjadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki, wengi wakiona kuwa ni onyo kwa wasanii chipukizi wawe makini na mikataba wanayosaini. Khaligraph ameendelea kujijengea jina kama msanii anayejitegemea kupitia lebo yake ya Blue Ink, huku akiendelea kung’ara ndani na nje ya Kenya.
Wakati baadhi ya mashabiki walimpongeza kwa msimamo wake, wengine walihisi kuwa sio rahisi kwa kila msanii kujisimamia bila msaada wa lebo kubwa. Hata hivyo, ujumbe wake umeibua mjadala mpana kuhusu changamoto za kifedha zinazowakumba wasanii licha ya umaarufu wao.