
Mwanamuziki maarufu wa Kenya, Victoria Kimani, amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kuwa hajawahi kutongozwa kimapenzi na mwanaume yeyote wa Kenya.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Kimani alisema kuwa licha ya kuwa mzaliwa na mzawa wa Kenya, wanaume kutoka taifa hilo hawajawahi kumwonyesha nia ya kimapenzi, na hata wanapojaribu, lugha yao ya ushawishi huwa haina mvuto.
“Wanaume wa Kenya hawajawahi kunitongoza. Na ikitokea, lugha yao ya kimapenzi haivutii kabisa,” alisema Kimani.
Ameongeza kuwa mara nyingi wanaume kutoka mataifa ya nje ndio humfuata kwa mapenzi, huku akieleza kuwa tofauti ya ujasiri na mbinu zao za ushawishi ni kubwa ikilinganishwa na Wakenya.
Victoria, ambaye amewahi kufanya kazi na wanamuziki wa kimataifa na kuishi katika mataifa mbalimbali, alisisitiza kuwa hana kinyongo na wanaume wa nyumbani, lakini anatamani kuona mabadiliko katika jinsi wanavyoonyesha mapenzi yao.
Kauli hiyo imeibua mjadala mkali mitandaoni, baadhi ya mashabiki wakimtetea huku wengine wakihisi kuwa anawadharau wanaume wa taifa lake. Wengine walihoji kuwa labda hofu ya umaarufu wake au hadhi yake ya juu ndiyo huwafanya wanaume wa Kenya kutojaribu kumtongoza.
Victoria Kimani ameendelea kuwa mmoja wa wasanii wa kike wa Kenya wanaotambulika kimataifa kutokana na sauti yake ya kipekee, mitindo ya kisasa, na ujasiri wa kusema anachohisi bila woga.