
Msanii nguli wa muziki wa Dancehall kutoka Jamaica, Vybz Kartel, ameonyesha nia ya dhati kutua nchini Kenya kwa ajili ya kutumbuiza.
Akiwa live kwenye Instagram, Kartel aliwapa mashabiki wake wa Kenya sababu ya kutabasamu baada ya kutoa wito kwa waandaaji wa matamasha nchini, akiwataka wamualike rasmi kwa tamasha kubwa.
“Tell promoters Kartel is ready to come home,” alisema Kartel kwa sauti ya msisitizo huku akionekana mwenye shauku ya kuwa karibu na mashabiki wake wa Afrika, hususan Kenya.
Kauli hiyo imeibua shangwe kubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa reggae na dancehall nchini Kenya, ambao wamekuwa wakimsubiri msanii huyo kwa muda mrefu. Katika ujumbe wake, Kartel alieleza mapenzi yake kwa Kenya, akiitaja kama “nyumbani”, jambo lililowasisimua wengi na kuongeza matumaini kuwa huenda onyesho lake nchini likawa karibu zaidi kuliko ilivyodhaniwa.
Hadi sasa, mashabiki tayari wameanza kuwataja waandaaji wakubwa wa matamasha kama Shoke Shoke Festival, Koroga Festival, Blankets & Wine, na OktobaFest, wakiwataka wachukue hatua za haraka kuhakikisha Vybz Kartel anakuja nchini.
Hii si mara ya kwanza msanii huyo kutuma ujumbe wenye mapenzi kwa bara la Afrika, lakini kutaja Kenya kwa jina na kuitambua kama nyumbani ni hatua ya kipekee inayodhihirisha ukubwa wa soko la muziki Afrika Mashariki na mapokezi mazuri anayopata kutoka kwa mashabiki wa eneo hili.