
Chelsea wametwaa Kombe la Dunia la Klabu 2025 kwa kishindo baada ya kuichapa Paris Saint-Germain (PSG) mabao 3-0 katika fainali iliyopigwa Julai 13 kwenye uwanja wa MetLife, New Jersey. Cole Palmer alifunga mabao mawili dakika ya 22 na 30, kabla ya João Pedro kuongeza la tatu dakika ya 43, na kuifanya Chelsea kutawala mchezo tangu mwanzo hadi mwisho.
Mchezo huo ulionyesha ubora mkubwa wa kikosi cha Chelsea kilicho chini ya kocha Enzo Maresca, huku PSG wakionekana kuzidiwa mbinu na kasi ya wapinzani wao. PSG walijikuta wakizidiwa katika kila idara na walionekana kukata tamaa mapema baada ya bao la tatu kabla ya mapumziko.
Dakika ya 83, PSG walipata pigo zaidi baada ya João Neves kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumvuta nywele beki Marc Cucurella wa Chelsea. Tukio hilo lilizua tafrani, huku kocha Luis Enrique akigombana na João Pedro wa Chelsea kwa madai ya kuchelewesha muda wakati wa mabadiliko.
Mechi hiyo pia ilihudhuriwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alimkabidhi nahodha wa Chelsea, Reece James, kombe hilo. Hata hivyo, kitendo hicho kilizua hisia tofauti kutoka kwa mashabiki waliomzomea Trump huku wengine wakimshangilia. Cole Palmer alitangazwa mchezaji bora wa mechi hiyo kwa mchango wake mkubwa.
Ushindi huo unakuwa wa pili kwa Chelsea kwenye historia ya Kombe la Dunia la Klabu, baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2021. Kwa ushindi huu, The Blues wamethibitisha kuwa wako katika njia sahihi ya kurejea kwenye kilele cha soka la dunia, wakiwa na kikosi kipya chenye njaa ya mafanikio.