Entertainment

Eddy Kenzo: Lugha Sio Kizuizi kwa Mafanikio ya Muziki wa Kimataifa

Eddy Kenzo: Lugha Sio Kizuizi kwa Mafanikio ya Muziki wa Kimataifa

Msanii nyota kutoka Uganda, Eddy Kenzo, amesema kuwa lugha haipaswi kuwa kikwazo kwa wasanii wanaotamani kupata mafanikio ya kimataifa katika tasnia ya muziki.

Akizungumza katika mahojiano yake hivi karibuni, Kenzo alisisitiza kuwa muziki ni lugha ya kipekee inayovuka mipaka ya maneno na kueleweka na watu wa mataifa tofauti duniani.

Eddy Kenzo, ambaye alitambulika kimataifa kupitia kibao chake Sitya Loss, alisema kuwa watu wengi hawakuelewa maneno ya wimbo huo, lakini waliweza kuupenda na kucheza kwa hisia, jambo linalothibitisha kuwa hisia na midundo vinaweza kuunganishwa na hadhira ya aina yoyote.

Kenzo, anawahimiza wasanii wa Kiafrika kujiamini na kuendeleza utamaduni wao kupitia sanaa, bila kujaribu kubadilisha lugha yao kwa ajili ya soko la kimataifa. Anasema kuwa dunia sasa iko tayari kukumbatia utofauti wa kitamaduni na kisanaa kutoka barani Afrika.

Kauli yake inakuja wakati muziki wa Afrika unazidi kuvuma duniani kupitia majina makubwa kama Burna Boy, Diamond Platnumz, Tyla, na Ayra Starr, ambao baadhi yao pia wanatumia lugha za asili katika nyimbo zao.