LifeStyle

Petra Awataka Vijana Kuacha Maudhui Yenye Aibu Mitandaoni

Petra Awataka Vijana Kuacha Maudhui Yenye Aibu Mitandaoni

Msanii wa muziki Petra ameibuka na ujumbe mzito unaosisitiza umuhimu wa maadili na uadilifu katika safari ya mafanikio, akisema kuwa mtu hahitaji kushiriki katika maudhui ya ngono au kupoteza utu wake ili kufanikiwa kwenye tasnia ya burudani.

Kupitia mitandao ya kijamii, Petra ameeleza kuwa kizazi kipya kinahitaji kuamini kuwa mafanikio ya kweli hayaji kwa njia za kudhalilisha utu. Ameeleza kuwa haijalishi kiwango cha umaarufu mtu alicho nacho kwa sasa, kilicho muhimu ni kusimama na ukweli, akiamini kuwa Mungu anaweza kukuinua bila kuingia kwenye maovu.

Kauli ya Petra imekuja baada ya watu wengi mitandaoni kuonekana kupuuzilia mbali wito wa Katibu wa Mazingira jijini Nairobi, Geoffrey Mosiria, aliyeshutumu vikali video ya mwanamitandao maarufu Alicia Kanini iliyosambaa mitandaoni na kubeba maudhui ya ngono. Mosiria aliitaja video hiyo kuwa hatari kwa maadili ya kijamii, akisema ni mfano mbaya kwa vijana, hasa wasichana wadogo.

Wito wake umeibua maoni tofauti mitandaoni, baadhi ya mashabiki wakimpongeza kwa kusimamia maadili, huku wengine wakihisi kuwa tasnia ya burudani inahitaji uhuru wa kujieleza.

Hata hivyo, mjadala huu unaonyesha wazi kuwa suala la maadili katika mitandao ya kijamii na sanaa linaendelea kuwa muhimu hasa kwa kizazi kipya kinachotegemea mtandao kama jukwaa la kuonyesha vipaji.