Entertainment

Konshens Afunguka Kuhusu Mvutano Wake na Mtayarishaji wa Muziki Rvssian

Konshens Afunguka Kuhusu Mvutano Wake na Mtayarishaji wa Muziki Rvssian

Msanii wa Dancehall kutoka Jamaica, Konshens, amezungumzia kwa mara ya kwanza mvutano wake na mtayarishaji maarufu wa muziki Rvssian, ambao umekuwa ukigonga vichwa vya habari.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Konshens amemtuhumu Rvssian kwa kusambaza taarifa potofu kuhusu mzozo wao na kufichua kuwa chanzo kikuu cha mgogoro huo ni masuala ya kifedha, siyo ukosefu wa uaminifu au urafiki.

Katika ujumbe wake, Konshens ameeleza kuwa alimtaka Rvssian alipe sehemu ndogo ya fedha zilizokuwa zinadaiwa kutokana na ushirikiano wao wa awali. Hata hivyo, badala ya kushughulikia suala hilo kwa mazungumzo, Rvssian alimu-unfollow kwenye mitandao ya kijamii. Konshens amekiri kwamba aliwahi kutishia kumpeleka mahakamani, lakini amekanusha madai kuwa aliwahi kumshtaki rasmi, akisema walimaliza tofauti zao nje ya mahakama.

Msanii huyo ameelezea kuwa hatua ya Rvssian kusambaza taarifa za uongo kwa umma ni usaliti mkubwa, akisisitiza kuwa alikuwa kama ndugu kwake.

Licha ya mzozo huo, Rvssian bado anatajwa kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Konshens. Wimbo wao wa pamoja wa mwaka 2016 “Privado”, una zaidi ya views milioni 294 kwenye mtandao wa YouTube, na kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya Konshens katika jukwaa la kimataifa.