Tech news

WhatsApp Kuleta Muhtasari wa Meseji Kupitia Teknolojia ya Akili Bandia

WhatsApp Kuleta Muhtasari wa Meseji Kupitia Teknolojia ya Akili Bandia

Kampuni ya Meta, inayomiliki WhatsApp, imetangaza kuwa inafanyia majaribio kipengele kipya cha akili bandia (AI) kitakachowezesha watumiaji wake kufupisha mazungumzo marefu kwenye meseji.

Kwa kutumia teknolojia ya AI, WhatsApp itawaruhusu watumiaji kupata muhtasari wa haraka wa mazungumzo yao, jambo ambalo linalenga kusaidia wale wanaopokea ujumbe mwingi au ambao hawakuwahi kufuatilia kila ujumbe mmoja mmoja.

Kipengele hiki kinatarajiwa kufanya kazi kwa kuchambua mazungumzo ya kundi au mtu binafsi, kisha kutoa muhtasari wa mambo muhimu yaliyojadiliwa, huku kikihifadhi usalama na faragha ya watumiaji kwa kutumia teknolojia ya usimbaji wa mwisho kwa mwisho (end-to-end encryption).

Taarifa kutoka kwa baadhi ya watumiaji waliopata toleo la majaribio zinasema kuwa kipengele hicho kiko chini ya sehemu ya “Chat Summary,” ambapo AI inaweza kutoa dondoo fupi kuhusu mazungumzo yaliyopita.

Hii ni moja kati ya hatua kadhaa ambazo Meta imeanza kuzitekeleza ili kuimarisha matumizi ya AI kwenye majukwaa yake, ikiwa ni pamoja na kuanzisha wasaidizi wa kidijitali ndani ya WhatsApp na Messenger.

Hadi sasa, Meta haijatoa tarehe rasmi ya kuachia kipengele hicho kwa watumiaji wote, lakini matarajio ni kuwa kitakuwa sehemu ya masasisho yajayo ya WhatsApp mwaka huu