Rapa mwenye utata, Toxic Lyrikali, amewajibu vikali wakosoaji wake mitandaoni wanaomuita msaliti, kufuatia hatua yake ya kumtawaza Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Nairobi.
Kupitia Instagram Live, msanii huyo amesisitiza kuwa hana muda wa kujibizana na wakosoaji, akieleza kuwa kwa sasa anataka kufurahia matunda ya kazi yake ya muziki..
Hitmaker huyo wa Backbencher, ameongeza kuwa hatatishwa na maneno ya kejeli dhidi yake, akieleza kuwa maisha ya tabu na raha yamekuwa sehemu ya safari yake ya muziki, hivyo hawezi kuyumbishwa na maneno ya wafuasi wake.
Aidha, rapa huyo amewataka wakosoaji wake kuacha kufuatilia maisha yake binafsi na badala yake wazingatie shughuli zinazoweza kuwapatia riziki.
Hata hivyo, msanii huyo kwa sasa anatuhumiwa na baadhi ya mashabiki kuwa na kiburi na pia kuwasaliti vijana, hasa kwa kuonyesha uhusiano wa karibu na serikali ya Rais Ruto, ambayo imekuwa ikikumbana na upinzani mkubwa hasa kutoka kwa vijana mitandaoni.