
Mwanahabari na mchambuzi wa michezo Fred Arocho amemtaka msanii Bahati kuhakikisha anatimiza ahadi alizotoa kwa wachezaji wa timu ya taifa, Harambee Stars.
Kwenye mahojiano na SPM Buzz, Arocho amesema ni lazima Bahati atimize wajibu huo badala ya kuwatumia wachezaji hao kama chombo cha kujitafutia umaarufu.
Katika ujumbe wake, Arocho alisisitiza kuwa pesa alizoahidi lazima zitolewe na si sawa kwa Bahati kutumia jina la Harambee Stars kupata kiki za kibinafsi huku wachezaji wakiwa hawajafaidika. Kauli hiyo imeibua mjadala mkali mitandaoni, mashabiki wengi wakimtaka Bahati kutoa ufafanuzi kuhusu iwapo atatimiza au atapuuza ahadi yake.
Bahati kwa upande wake bado hajatoa majibu ya moja kwa moja kuhusu shinikizo hilo, lakini mashabiki wa kandanda wameungana na Arocho wakisema heshima ya wachezaji wa taifa inapaswa kupewa kipaumbele na si kutumiwa kama daraja la kujitafutia umaarufu.
Mjadala huu unaendelea kushika moto, huku macho yote yakielekezwa kwa Bahati ili kuona kama atatekeleza ahadi zake au la.