
Kampuni ya teknolojia ya Meta imeanzisha majaribio ya mfumo mpya unaoweza kuchanganua picha zilizohifadhiwa kwenye simu za watumiaji ili kumpa ushauri wa content wanazoweza kutengeneza. Mfumo huo unadaiwa kuwa na uwezo wa kutambua sura za watu, maeneo, vitu na hata aina za picha zilizopo kwenye kifaa cha mtumiaji.
Kwa kutumia taarifa hizo, Meta inalenga kuwasaidia watumiaji wake kupata mawazo ya haraka ya post au video kulingana na maisha yao ya kila siku. Hii inamaanisha kuwa picha binafsi zinaweza kuwa msingi wa mapendekezo ya content mpya kwenye Instagram, Facebook au Threads.
Hata hivyo, hatua hii imeibua mjadala kuhusu faragha na usalama wa data binafsi. Wataalamu wa teknolojia wameonya kuwa kukagua na kutuma picha binafsi hadi kwenye seva za Meta kunaweza kusababisha hofu kwa watumiaji, hasa kutokana na uwezekano wa matumizi mabaya ya taarifa hizo.
Meta haijatoa maelezo ya kina kuhusu jinsi mfumo huu utavyolinda faragha za watumiaji, lakini imeeleza kuwa inalenga kuboresha ubunifu na uhusiano wa watu na mitandao yake ya kijamii. Ikiwa utatekelezwa kikamilifu, mfumo huu unaweza kubadilisha kwa kiwango kikubwa namna content inavyoundwa mtandaoni.