Msanii Nyota Ndogo ametoa ujumbe mzito kwa wasichana wa Kiafrika wanaofanya kazi katika mataifa ya Kiarabu, akiwataka kuwa waangalifu na mahusiano ya mtandaoni. Kupitia Instgram yake, ameeleza kuwa mabinti wengi hujikuta wakitumika kihisia na kifedha na wanaume wasiowajali, huku wakiteseka kazini kwa masharti magumu.
Nyota Ndogo amesema kuwa baadhi ya wanaume huwatumia wanawake walioko nje ya nchi kama chanzo cha fedha, wakiwadanganya kwa maneno matamu ya mapenzi. Amesema wapo wanaume wanaowalazimisha wanawake kuwatumia pesa za kodi, miradi au matumizi ya kila siku, huku wao wakifaidika kwa urahisi bila kuchangia chochote.
Akiwa na uzoefu binafsi wa kufanya kazi ya ndani akiwa na umri wa miaka 17, Nyota amesema anafahamu vyema uchungu wa maisha ya ughaibuni. Alisisitiza kuwa wanawake wengi hujikuta wakibeba mzigo mara mbili kazi ngumu na mahusiano yenye mateso ya kihisia.
Hitmaker huyo wa Watu na Viatu, ameonya kuwa tabia hii imewafanya baadhi ya wanaume kuwa wavivu wa maisha, kwa sababu wanategemea msaada kutoka kwa wanawake walioko nje. Alishauri mabinti wajifunze kujipenda na kutosema kila kitu mtandaoni, kwani baadhi ya watu hutumia taarifa hizo kuwadhulumu.
Nyota Ndogo amemalizia kwa kuwaombea wasichana walioko ughaibuni, akisisitiza kuwa wanahitaji ulinzi wa Mungu dhidi ya udanganyifu wa mapenzi na hali ngumu za kazi. Kauli yake imeibua hisia mbalimbali mitandaoni, wengi wakikiri kuguswa na ujumbe huo wa uhalisia.