
Mshambulizi wa Harambee Stars Ryan Ogam amekamilisha uhamisho wake kujiunga na kilabu cha Wolfsberger AC cha Austria kutoka kilabu cha Tusker FC kinachoshiriki katika ligi kuu ya FKF.
Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye alijipatia umaarufu kwa kufunga mabao mawili kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, atajiunga na wachezaji wenzake wapya baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Ogam alikuwa mmoja wa wachezaji bora wa Ligi Kuu ya FKF msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 15 katika mechi 17 pekee za Tusker FC. Wolfsberger, ambayo ilimaliza katika nafasi ya nne katika ligi ya Bundesliga ya Austria msimu uliopita, imemsajili mshambulizi huyo ili kuboresha safu yao ya ushambulizi. Uhamisho wake unaashiria sura mpya katika taaluma yake ya soka, na kumpa jukwaa jipya la kujipima nguvu katika soka la bara Ulaya.