Mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Rwanda, Gloriose Musabyimana maarufu kama Gogo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 36.
Taarifa zinaeleza kuwa Gogo alifariki usiku wa Septemba 3, 2025 nchini Uganda baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kifo chake kimewashtua mashabiki na wadau wa muziki, ambapo wengi wameeleza masikitiko yao kupitia mitandao ya kijamii.
Gogo alipata umaarufu kupitia nyimbo zake za injili mtandaoni, hususan wimbo wake “Blood of Jesus Christ”, uliomuwezesha kupata mashabiki wengi wa muziki wa injili. Nyimbo zake za kuinua roho zilimfungulia milango ya kutumbuiza katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Uganda ambako aliwahi kushiriki katika Mega Gospel Concerts.
Hivi karibuni, aliwahi kufanya onyesho mjini Mbarara, na wakati wa kifo chake alikuwa bado jijini Kampala, Uganda. Ingawa chanzo halisi cha kifo chake bado hakijabainika, taarifa zinaashiria kuwa alikumbwa na changamoto kadhaa za kiafya kabla ya mauti.
Msanii Bruno K, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Gogo, amethibitisha taarifa za kifo chake kupitia mtandao wa kijamii leo asubuhi kwa huzuni kubwa.
“Ni habari za kusikitisha kweli,” aliandika. “Nilipigiwa simu leo asubuhi kuarifiwa kuhusu kifo cha Gogo. Ni kweli ameenda kukutana na Bwana; meneja wake ndiye aliyenithibitishia.”
Kifo cha Gogo kimeacha pengo kubwa katika muziki wa injili, huku mashabiki na wenzake wakimkumbuka kwa sauti yake yenye nguvu na ujumbe wa matumaini aliouacha kupitia muziki.