Mshawishi wa mitandaoni kutoka Kenya, Kelvin Kinuthia, amewashangaza mashabiki wake baada ya kutangaza kuwa ana mpango wa kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza mfuko wa uzazi (Uterus Transplant – UTX). Hii ni aina ya upasuaji wa kibingwa ambapo mfuko wa uzazi kutoka kwa mtoaji (donor) hupandikizwa kwa mpokeaji ili kumpa uwezo wa kubeba mimba
Kupitia ukurasa wake wa Instagram ameeleza kwamba maisha yake ni ya faragha na hakuna aliyekuwa akifahamu mipango yake ya kufanyiwa upasuaji huo. Amesema amekuwa akipitia maandalizi ya kimatibabu kwa muda mrefu na amejiandaa kisaikolojia kwa safari hiyo.
Pia amefafanua kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu anaamini kila mtu ana haki ya kuwa na familia na kupata mtoto, na ana matumaini makubwa kuwa teknolojia ya kisasa ya tiba itamwezesha kutimiza ndoto hiyo.
Kwa mujibu wa Kinuthia, uamuzi wake wa kuzungumzia suala hilo hadharani unatokana na dhamira ya kuwapa ujasiri watu wengine wanaopitia changamoto za kiafya au wale wanaotamani kupata watoto kwa njia zisizo za kawaida.
Uterus transplant ni miongoni mwa upasuaji wa hali ya juu unaofanyika mara chache duniani na umewezesha wanawake waliokuwa hawana uwezo wa kubeba ujauzito kupata nafasi ya kujifungua watoto wao wenyewe. Hata hivyo, upasuaji huu unahitaji maandalizi ya kina, usimamizi wa madaktari bingwa, na dawa maalum za kuzuia mwili kukataa kiungo kilichopandikizwa.