
Msanii wa nyimbo za injili Daddy Owen ameibua mjadala baada ya kutoa kauli yenye kugusa hisia kuhusu ndoa na changamoto za talaka.
Akizungumza kwenye mahojiano, msanii huyo amesema kuwa kwa mtazamo wake, ni rahisi zaidi mtu kukubali kifo cha mpendwa wake kuliko kukabiliana na talaka, hasa pale ambapo kuna watoto.
Kwa mujibu wa Daddy Owen, talaka huacha jeraha refu kwa sababu yule uliyeachana naye ataendelea kuwepo kwenye maisha yako kupitia majukumu ya malezi. Msanii huyo ameongeza kuwa hali huwa ngumu zaidi endapo bado kuna hisia za kimapenzi kwa mtu huyo, jambo linalomfanya aliyeachika kupata wakati mgumu zaidi kisaikolojia na kihisia.
Kauli hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti miongoni mwa mashabiki na wafuasi wake. Wapo waliomuunga mkono wakisema imani na uzoefu wake unaonyesha uhalisia wa maisha ya kifamilia, huku wengine wakihisi kuwa kulinganisha kifo na talaka ni jambo zito na tata.
Daddy Owen amekuwa wazi mara kadhaa kuhusu changamoto za maisha yake ya kifamilia na imani yake katika dini, na mara nyingi hutumia hadithi zake binafsi kutoa mafunzo kwa jamii.