
Msanii Stevo Simple Boy, ameamua kuzitumia ipasavyo pesa anazozikeshea na kuzitolea jasho baada ya kufanikisha hatua ya kuruka kwa ndege kwa mara ya kwanza. Safari hiyo haikuwa ya kawaida, kwani alichagua kumpeleka mpenzi wake mjamzito kwenye likizo maalum huko Diani.
Kupitia mitandao ya kijamii, Stevo alishiriki picha na video wakila bata, wakiburudika katika mandhari mazuri ya ufukweni huku wakionesha furaha na mapenzi ya dhati. Wawili hao walionekana wakifurahia chakula, vinywaji, na wakishikana mikono wakiwa ufukweni, huku wakifurahia mandhari ya bahari na upepo mwanana wa Diani.
Furaha ya Stevo na mkewe imeibua mjadala mtandaoni, mashabiki wengi wakimpongeza kwa kuthamini mpenzi wake mjamzito na kuchukua muda wa kuonyesha heshima na mapenzi mbele ya umma. Wengine walieleza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona msanii anayekulia mitaani sasa akifikia hatua ya kuonja raha ya maisha kupitia bidii yake ya muziki.