
Mwanamuziki wa Uganda, Weasel Manizo, na mkewe Sandra Teta wamejikuta tena katika mzozo mkali, miezi miwili tu baada ya tukio la awali ambapo inadaiwa Teta alimgonga kwa gari. Tukio jipya limeibuka kupitia video iliyosambaa usiku wa kuamkia jana, ikimuonyesha Weasel akiwa katika hali ya taharuki huku akilia akiomba msaada.
Katika video hiyo, Teta anaonekana akijaribu kumshambulia Weasel kwa kifaa kikali, wakati ndugu wa familia wakijitahidi kumzuia. Ingawa Teta alisikika akikanusha kumdhuru mumewe, bado haijabainika chanzo cha mzozo huo mpya. Weasel, akionekana mwenye hofu kubwa, alimshutumu mkewe kwa kumtesa na kumtaka aondoke nyumbani kwake, akisema hana tena amani naye.
Hali hii imewafanya mashabiki na wadau wa muziki kuhoji mustakabali wa ndoa yao, hasa ikizingatiwa kuwa si mara ya kwanza wawili hawa kuingia katika ugomvi wa hadharani.
Mnamo Julai mwaka huu, Teta alidaiwa kumgonga Weasel kwa gari katika baa moja eneo la Munyonyo, tukio lililosababisha msanii huyo kulazwa katika Hospitali ya Nsambya akiwa na mguu uliovunjika. Teta alikamatwa na polisi, lakini aliachiwa baada ya Weasel kuamua kutofungua mashtaka dhidi yake.