
Mwanamuziki nyota kutoka Nigeria, Tiwa Savage, amekanusha uvumi ulioenea kwa muda mrefu kwamba aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii mwenzake, Wizkid.
Akizungumza katika mahojiano na The Breakfast Club, Tiwa Savage amesisitiza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote. Ameeleza kuwa hakuwahi kuwa kwenye mahusiano ya siri na Wizkid na kuongeza kwamba maneno hayo ni uvumi wa watu usio na msingi.
Msanii huyo amefafanua kuwa madai hayo yalianza kuenea baada ya yeye kudaiwa kuwa kwenye uhusiano na mtu maarufu ambaye alitaka penzi lao libaki la siri. Hata hivyo, Tiwa amesema hana chochote cha kuficha na hakuwahi kushirikiana kimapenzi na Wizkid, bali walihusiana tu kwa sababu ya kazi za muziki.
Tiwa Savage, ambaye ni mmoja wa wasanii wa kike wenye ushawishi mkubwa barani Afrika na duniani, ameongeza kwamba anataka mashabiki wake waendelee kumtambua kupitia kazi zake na mafanikio ya muziki badala ya skendo za maisha yake ya kibinafsi.