
Rapa kutoka Tanzania, Rosa Ree, amehoji mienendo ya baadhi ya wasanii wa muziki ambao bado wanaendelea kutoa nyimbo za mapenzi katika kipindi ambacho taifa lipo kwenye joto la uchaguzi.
Mkali huyo wa ngoma ya Sauti za Maskini, amesema kuwa, kwa sasa wasanii wanapaswa kutumia nafasi yao kuelimisha na kuibua mijadala yenye manufaa kwa jamii, badala ya kuwekeza nguvu zao katika muziki wa mapenzi pekee.
Rosa Ree ameongeza kuwa mara nyingi wasanii huwa na nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo ya vijana na jamii kwa ujumla, hivyo inashangaza kuona wengi wao wakipuuza majukumu hayo muhimu.
Kwa mujibu wake, hali hii imemfanya afikirie upya nafasi yake kama msanii, akidai hata amewahi kujuta kwa uamuzi wake wa kuingia kwenye tasnia ya muziki nchini Tanzania. Ameeleza kuwa sanaa ni silaha kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha jamii, hasa inapokaribia kipindi muhimu cha kisiasa.