Mchekeshaji na mwanaharakati wa kijamii kutoka Kenya Eric Omondi ameanzisha rasmi kampeni ya kitaifa yenye lengo la kuhamasisha vijana wa kizazi cha Gen Z kujisajili kama wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Kupitia hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi, Eric amesema kuwa kampeni hiyo ni ya kihistoria kwa taifa la Kenya kwani inaashiria mwanzo wa safari ya kuleta mabadiliko ya kisiasa kupitia ushiriki wa vijana.
Omondi ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kutembelea vyuo vikuu vyote nchini humo ili kuhakikisha vijana wanatumia haki yao ya kidemokrasia kwa kujisajili na kushiriki katika uchaguzi.
Mchekeshaji huyo, amesisitiza kuwa ni wakati wa vijana kuamka na kubeba jukumu la kuunda taifa jipya kupitia kura zao, akiahidi kutembelea kila pembe ya Kenya ili kuhakikisha “Kenya Mpya” inajengwa na vijana wenye ari ya mabadiliko.
Eric Omondi, ambaye kwa miezi ya hivi karibuni amekuwa akijitokeza kama sauti ya vijana katika masuala ya kijamii na kiuchumi, amesema anaamini kuwa nguvu ya vijana ndiyo nguzo kuu ya mabadiliko nchini humo.