Msanii wa muziki kutoka Kenya, Bahati, ameomba radhi hadharani baada ya kuzua mjadala mkubwa mtandaoni kufuatia ujumbe wa picha ya mazungumzo (screenshot) aliouchapisha wakati akiomboleza kifo cha msanii wa Gengetone, Shalkido.
Kupitia Instagram, Bahati ametoa ufafanuzi akisema ujumbe huo ulieleweka vibaya na kwamba mawasiliano hayo yalikuwa kati ya Shalkido na timu yake ya usimamizi, si yeye binafsi. Ameongeza kuwa hakumpuuza Shalkido kwani alikuwa amepanga kurekodi nyimbo kadhaa za ushirikiano na wasanii wengine, ikiwemo ule aliokuwa amepanga kufanya na marehemu.
Bahati pia amesema kuwa anaamini baadhi ya wakosoaji wake wanaendelea kumshambulia kwa sababu bado wana machungu naye kutokana na wimbo wake wenye utata, Seti, ambao uliibua hisia kali na mijadala mikubwa mtandaoni.
Hata hivyo amesisitiza kuwa hajawahi kuwa na nia mbaya, akiwataka mashabiki wake kuelewa kuwa alikuwa akiomboleza msanii aliyekuwa rafiki na kwamba post yake haikukusudiwa kuleta tafsiri mbaya.
Kauli ya Bahati imekuja baada ya mashabiki kumshambuli vikali mtandaoni wakidai alimpuuza msanii huyo kabla ya kifo chake, wakimtuhumu kutumia tukio hilo kujitafutia kiki.