Msanii wa Bongo Fleva Chino ameibua gumzo mitandaoni baada ya kuchapisha ujumbe wa hisia kali kufuatia tangazo la Mdogo Sajent kwamba hatofanya tena kazi na kundi la Wanaman Gang.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chino ameonyesha wazi maumivu na hisia za usaliti akisema kuwa mara nyingine mtu anaweza kuwa na roho nzuri, lakini bado akafanyiwa roho mbaya na binadamu.
Dansa huyo aliyegeukia muziki, ameeleza kushangazwa na hatua ya Mdogo Sajent kuondoka licha ya msaada na jitihada alizowahi kumpa, akiongeza kuwa kitendo hicho kimemuumiza sana na kimemfanya kuamini kuwa binadamu wana maudhi.
Hata hivyo, mashabiki mitandaoni wameanza kutilia shaka tukio hilo, wakidai kuwa huenda ni kiki iliyopangwa kimkakati ili kuvutia umakini wa mashabiki kabla ya kuachia kazi mpya.
Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na wasanii hao zinaeleza kuwa mvutano wao ulianza kutokana na tofauti za kimanagement na malalamiko kuhusu ushirikiano na uongozi ndani ya kundi hilo.