Timu ya taifa ya raga ya Kenya, Shujaa, inatarajiwa kuanza rasmi kampeni yake ya kutetea ubingwa wa mashindano ya mwaka huu ya Safari Sevens kwa kuchuana na timu ya Walukuba Rugby kwenye mechi ya ufunguzi itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo jijini Nairobi.
Baada ya mechi hiyo, Shujaa itavaana na UK Select kisha kumalizia mechi za makundi kwa kupimana nguvu na timu ya French Renegades kesho.
Timu nyingine ya Kenya kwenye mashindano hayo, Morans, nayo itaanza harakati zake kwa kukutana na Re-Union, kabla ya kupambana na Apache na Zimbabwe katika michezo mingine ya hatua ya makundi.
Kwa upande wa wanawake, timu ya taifa ya Kenya Lionesses itaanza kampeni yake kwa kucheza dhidi ya Tunisia, kisha kuchuana na Ubelgiji kabla ya kumalizia hatua ya makundi dhidi ya Uganda.
Katika hatua nyingine, Benki ya KCB imetangaza kudhamini mashindano ya mwaka huu kwa kutoa msaada wa shilingi milioni 4.5 kama sehemu ya mchango wao kwa ukuzaji wa michezo nchini. Timu ya KCB RFC, ambayo imeshinda msururu wa raga wa ndani kwa msimu huu, pia itashiriki kwenye Safari Sevens na itaanza kwa kumenyana na timu ya Shogun, iliyomaliza katika nafasi ya pili mwaka jana.
Mashindano ya Safari Sevens kwa mwaka huu yamevutia timu 20 za wanaume na 8 za wanawake kutoka mataifa mbalimbali, hali inayotarajiwa kuongeza ushindani na burudani ya hali ya juu kwa mashabiki wa mchezo wa raga.