Msanii chipukizi wa muziki kutoka Kenya, Angel Atieno, ameipa nchi yake heshima kubwa baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye shindano maarufu la Our Generation Singing Competition lililofanyika nchini Urusi.
Shindano hilo lilileta pamoja vijana wenye vipaji vya muziki kutoka nchi 16, ambapo binti huyo mwenye umri wa miaka 12 aling’aa kupitia wimbo wake wa asili uitwao Nyota.
Uimbaji wake wenye hisia na uhalisia ulimvutia majaji na mashabiki, na kumpa nafasi ya kuorodheshwa miongoni mwa sauti changa bora barani Afrika, hatua muhimu katika safari yake ya kimuziki.
Angel alianza kujulikana mwaka 2020, kipindi cha COVID-19, alipoanza kushiriki cover za nyimbo maarufu kwenye mitandao ya kijamii. Sauti yake laini na ya kuvutia ilimletea umaarufu mkubwa, na kufanikisha kupata zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye TikTok na Facebook.
Umaarufu huo ulimfungulia milango ya uigizaji, ambapo alipata nafasi katika tamthilia ya “Zora” iliyoruka kupitia Citizen TV kati ya mwaka 2021 na 2022, chini ya utayarishaji wa Lulu Hassan.
Kwa sasa, Angel ni mwendeshaji wa kipindi cha watoto cha G3 Kids Show kinachoruka NTV Kenya, sambamba na kazi yake kama voice over artist lakini pia msanii wa kurekodi nyimbo.