Entertainment

Wasanii wa Uganda Wamlilia Raila Odinga, Wamtaja Kama Shujaa wa Afrika

Wasanii wa Uganda Wamlilia Raila Odinga, Wamtaja Kama Shujaa wa Afrika

Kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Amolo Odinga, kimegusa hisia za wasanii nchini Uganda, wakiongozwa na Jose Chameleone na Bobi Wine, ambao wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na wananchi wa Kenya.

Kupitia Instagram, msanii nyota Jose Chameleone amemtaja Raila kama kiongozi aliyewaunganisha watu wa Afrika Mashariki kupitia siasa, utu, na msimamo wake wa kupigania demokrasia. Chameleone amesema Afrika Mashariki imepoteza kiongozi wa kipekee aliyekuwa mfano wa ujasiri na upendo kwa watu wake.

Kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, naye kupitia ujumbe wake katika mtandao wa X, amemsifia Raila kama kiongozi ambaye kwa miongo kadhaa alibaki kuwa sauti ya matumaini kwa waliodhulumiwa na aliyetetea haki za watu kwa ujasiri usioyumba.

Wasanii wengine kutoka Uganda, akiwemo Eddy Kenzo, Sheebah, Spice Diana, na King Saha, pia wametuma salamu za rambirambi wakisisitiza kuwa Raila alikuwa kiongozi wa watu wote na alichangia kujenga uhusiano wa karibu kati ya Kenya na Uganda.

Hata hivyo katika salamu zao za pole, wasanii hao kwa pamoja wametuma rambirambi kwa Mama Ida Odinga, familia ya Raila, na wananchi wote wa Kenya, wakiwatia moyo waendelee kudumisha maono na urithi wa kiongozi huyo.

Salamu hizo kutoka Uganda zimepokelewa kwa heshima kubwa na Wakenya, wengi wakisifia umoja wa kikanda ulioonekana katika maombolezo haya, wakisema Raila Odinga ataendelea kukumbukwa kama Baba wa Mapambano na mwanamageuzi wa kweli wa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *