Staa wa muziki nchini Kenya, Willy Paul, ametoa wito kwa serikali kuanzisha siku maalum ya kitaifa iitwayo “Raila Odinga Day” na kusimika sanamu ya kiongozi huyo Jijini Nairobi kama ishara ya heshima kwa mchango wake mkubwa kwa taifa.
Kupitia ujumbe alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Willy Paul amesema hatua hiyo itakuwa njia bora ya kudumisha urithi wa kisiasa na kijamii wa aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Raila Amolo Odinga, ambaye amekuwa nembo ya mapambano ya demokrasia nchini Kenya kwa zaidi ya miongo mitatu.
Wito wa Willy Paul unakuja wakati taifa linaendelea kuomboleza kifo cha kiongozi huyo mashuhuri, ambaye alizikwa jana katika nyumba yake ya milele huko Bondo, kaunti ya Siaya.
Endapo pendekezo hilo litatekelezwa, “Raila Odinga Day” itakuwa miongoni mwa siku za kitaifa zinazoheshimu viongozi waliotoa mchango mkubwa kwa taifa, huku sanamu yake katikati ya jiji la Nairobi ikitarajiwa kuwa alama ya kumbukumbu na heshima ya kizazi kijacho.