 
									Mfalme wa rap nchini Kenya, Khaligraph Jones, amedokeza uwezekano wa kufanya kolabo na msanii anayechipukia kwa kasi, Toxic Lyrikali, huku akimsifia kwa kuendelea kushikilia mizizi ya rap nchini humo.
Kupitia mazungumzo yaliyowekwa wazi na mdau wa muziki Thithad3, Khaligraph ameonyesha kuvutiwa na kazi ya Toxic, akisema kuwa kwa sasa ndiye anayeshikilia uhalisia wa rap nchini humo. Ameongeza kuwa iwapo watashirikiana kwenye wimbo, itakuwa ni kwa muda muafaka bila presha wala haraka.
Iwapo kolabo hiyo itatimia, itakuwa moja ya ushirikiano unaosubiriwa kwa hamu zaidi katika muziki wa hip hop wa Kenya mwaka huu.
Toxic Lyrikali, ambaye amekuwa akipata umaarufu kutokana na mtindo wake wa uandishi wa mashairi makali na uhalisia wa mitaani, anaendelea kutajwa kama mmoja wa wasanii wanaochukua nafasi kubwa katika kizazi kipya cha muziki wa hip hop nchini Kenya.
 
								 
             
             
                             
                             
                             
                             
                             
                             
                            