Msanii wa muziki kutoka Tanzania, Billnass, amejiondoa kwa muda kwenye mtandao wa Instagram kufuatia tukio la kuchomwa kwa duka lake la vifaa vya kielektroniki wakati wa maandamano yaliyoshuhudiwa nchini humo ya kupinga uchaguzi wa Oktoba 29.
Chanzo cha karibu na msanii huyo kimeeleza kuwa ameamua kuchukua mapumziko kutoka mitandaoni ili kujituliza kiakili na kushughulikia hasara kubwa iliyotokana na tukio hilo.
Duka lake, lililokuwa likiuza vifaa vya kielektroniki na muziki, liliharibiwa kabisa na moto uliowekwa na waandamanaji waliokuwa wakipinga hali ya kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania.
Inadaiwa kuwa Billnass alikuwa miongoni mwa wasanii waliowahi kuonyesha uungaji mkono kwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni, jambo ambalo limezua maoni mseto miongoni mwa Watanzania hasa katika kipindi hiki ambapo idadi kubwa ya wananchi inaonekana kupinga uongozi wake.