Mwanablogu, Murugi Munyi, amewashauri Wakenya kuwa wabunifu zaidi wanapowapa watoto wao majina, akisema majina kama Ethan, Jayden, na Michelle sasa yamezoeleka sana nchini humo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Murugi amesema kuwa ni wakati wazazi wa kizazi kipya wawe na ubunifu zaidi badala ya kurudia majina yale yale ambayo yamekuwa yakitumika kwa miongo kadhaa.
Ameongeza kuwa mwaka 2025 unatoa fursa nyingi kwa wazazi, kwani sasa kuna mtandao na zana za kisasa za akili bandia (AI), ambazo zinaweza kuwasaidia kutafuta mawazo mapya na ya kipekee ya majina.
Kauli yake imezua mjadala mtandaoni, baadhi ya Wakenya wakikubaliana naye kuwa ubunifu ni muhimu katika utambulisho wa watoto, huku wengine wakisema wazazi wanapaswa kuwa na uhuru wa kuchagua majina wanayoyapenda bila kuhukumiwa.