Mtangazaji maarufu wa Tanzania Mwijaku ameomba radhi kwa Watanzania kwa kusimama na kuunga mkono serikali wakati wa kampeni za uchaguzi wa Oktoba 29.
Kupitia sauti iliyosambaa mitandaoni, Mwijaku amesema anatambua kuwa baadhi ya kauli zake wakati wa kampeni ziliwaumiza wananchi, hasa ikizingatiwa machafuko yaliyofuata baada ya uchaguzi huo.
Amesema lengo lake halikuwa kuwagawanya Watanzania bali kuhimiza amani na umoja, na sasa anawataka wananchi kuachana na lawama na badala yake kuelekeza nguvu katika kujenga taifa upya.
Kauli ya Mwijaku imepokewa kwa hisia mseto mitandaoni, baadhi wakimsifu kwa ujasiri wa kukiri makosa yake, huku wengine wakimtaka aende mbali zaidi kwa kutumia sauti yake kuwatetea wananchi wanaodaiwa kuuwawa kutokana na vurugu za baada ya uchaguzi.