Shirikisho la Soka barani Afrika CAF limethibitisha kuwa Tuzo za mwaka huu za CAF zitaandaliwa mjini Rabat, Morocco. Sherehe hizo za kila mwaka huwatuza wachezaji, makocha na timu mashuhuri ambazo zimeandikisha matokeo mazuri katika soka la Afrika katika msimu uliopita.
Tuzo hizo ambazo huchukuliwa kuwa moja ya hafla za kifahari zaidi kwenye kalenda ya soka barani Afrika, huwaleta pamoja nyota wa soka barani Afrika pamoja na wachezaji wa kimataifa. Miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo hiyo kwa wanaume ni Achraf Hakimi wa Morocco, Mohamed Salah wa Misri, na Victor Osimhen wa Nigeria.
Kwa upande wa wanawake, Barbra Banda wa Zambia anaongoza orodha ya walioteuliwa ambayo pia inawajumuisha wachezaji wa kimataifa wa Morocco, Ghizlane Chebbak na Sanaa Mssoudy, ambao wote wamevutia na uchezaji wao kwenye jukwaa la kimataifa.