Mchekeshaji kutoka Kenya Flaqo ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kutoa maoni yake kuhusu wimbi la wasanii na wanamitindo wanaofanyiwa au kutangaza kufanyiwa upasuaji wa kuongeza maumbo, maarufu kama BBL (Brazilian Butt Lift).
Kupitia mitandao yake kijamii, ameeleza wazi mshangao wake kuhusu jinsi upasuaji wa BBL umeongezeka mno katika siku za hivi karibuni miongoni mwa mastaa wa kike. Amesema kuwa kwa sasa kila mahali anapogeukia kuna taarifa mpya za mtu kufanya au kupanga kufanya BBL, hali ambayo kwake inaibua maswali kuhusu nini hasa kinachochochea mwelekeo huo.
Flaqo, ambaye mara nyingi hutumia vipande vya ucheshi kuzungumzia masuala ya kijamii kama shinikizo la urembo, mitazamo ya watu kuhusu miili, na tabia za mtandaoni, ameongeza kuwa wimbi hili linachanganya kwa sababu linaonekana kuenea haraka kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Katika kipindi cha miezi kadhaa, mastaa wengi wa kike wamekuwa wakitangaza wazi kufanyiwa au kutafuta BBL, jambo ambalo limezua maoni tofauti mitandaoni. Wapo wanaosema ni uhuru wa mtu kubadili mwili wake, huku wengine wakihofia kuwa mwenendo huu unawaathiri hasa vijana wanaotazama mastaa kama mifano ya kuigwa.