Msanii aliyegeukia muziki wa mugithi, Peter Miracle Baby, amefunguka kwa uchungu namna msanii KRG The Don alivyodhalilisha mtandaoni kwa maneno makali kipindi ambacho afya yake ilikuwa imedhoofika.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Peter amesema kuwa alikuwa mlegevu na amelala kitandani hospitalini wakati KRG alipotumia maneno yaliyomuumiza kihisia na kumuathiri kisaikolojia. Amedai kuwa kipindi hicho alikuwa hana nguvu za kujibu wala kujitetea, jambo lililomfanya kuyaona maneno hayo kuwa ya kikatili na yasiyo na huruma.
Hata hivyo, licha ya kukerwa na tukio hilo, msanii huyo amesema tayari amemsamehe KRG, akiwataka mashabiki waache kuendeleza uhasama au malumbano. Amefafanua kuwa hataki kubeba chuki kwa sasa kwani anataka kuzingatia afya na maendeleo ya maisha yake binafsi.
Peter Miracle Baby ametoa kauli hiyo baada ya wafuasi wake kupuuzilia mbali azma ya KRG The Don ya kuwania kiti cha Useneta kaunti ya Nairobi kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2027 nchini Kenya. Wengi walidai kuwa msanii huyo hana sifa ya kuwa kiongozi kwa kutokana na mienendo yake ambayo wametaja kuwa ya kijeuri.