Mshawishi wa mitandao ya kijamii, anayejulikana kama Billionaire Chief Godlove, ameibua ghadhabu na mjadala mkali baada ya kuchapisha ujumbe wenye utata uliojaa dharau na kejeli dhidi ya wafuasi wake wanaohoji kuhusu utajiri wake.
Katika ujumbe huo uliowekwa kwenye mtandao wa Instagram, mwanamitandao huyo ameonekana kuwadharau wafuasi wake, akijibu maswali ya mara kwa mara kuhusu chanzo cha pesa zake kwa madai kuwa utajiri ni sehemu ya utambulisho wake wa asili na si jambo analolitafuta au kulifanyia kazi mahali pengine.
Godlove amewapa tahadhari wanaomkosoa, akiwataka kupunguza wivu, hasira, na mihemko isiyo na msingi. Ameeleza wazi kwamba wengi wanaomkosoa hawana msingi wa kufanya hivyo kutokana na hali zao duni za kiuchumi, kauli ambazo zimewafanya baadhi ya wafuasi kuhisi amewazungumzia kwa dharau kubwa na kuwaita maskini.
Sanjari na hilo, amechochea mjadala kwa kuwaambia wafuasi wake waweke akaunti zao ili awape pesa, akionyesha mtazamo wa kuwadhihaki wale anaodai kuwa wanapitia changamoto za kifedha.