Msanii nyota wa Uganda, Cindy, ameweka wazi kuwa hatajihusisha na kampeni za urais zinazondelea nchini humo kwa ajili ya kuilinda brand yake ya muziki na umoja wa mashabiki.
Akizungumza kwenye kituo kimoja cha runinga nchini humo, rais huyo wa Chama cha Wasanii nchini Uganda (UMA) amesema ameijenga taaluma yake kwa takriban miaka 20, na kwa mantiki hiyo hawezi kufanya uamuzi utakaowagawanya mashabiki wake.
Kwa mujibu wa Cindy, siasa ina asili ya kuleta mgawanyiko, na msanii anapoweka wazi kumuunga mkono mgombea fulani, huwa anapoteza sehemu kubwa ya mashabiki ambao hawapo kwenye upande huo.
Cindy sasa anaungana na wasanii kama Sheebah, Winnie Nwagi, na Azawi ambao wameamua kusimamisha ushiriki wao katika siasa ili kulinda ushawishi wao na hadhi ya kazi zao.
Hata hivyo, baadhi ya majina makubwa katika burudani kama Bebe Cool, Eddy Kenzo, na Jose Chameleone bado wanaonekana kuunga mkono mrengo wa Rais Yoweri Museveni, huku King Saha, Pallaso, na Fik Fameica wakisimama imara katika kambi ya Bobi Wine.