Mdau na mchambuzi wa masuala ya burudani kutoka Tanzania, El Mando, amesema kuwa mashabiki hawana uwezo wa kuushusha muziki wa Bongo Fleva, akisisitiza kuwa muziki huo umejengwa na kupiganiwa kwa muda mrefu na wadau wengi.
Akipiga stori na Bongoplus, El Mando amesema misukosuko ya kisiasa na mijadala ya mitandaoni haiwezi kuuangamiza muziki ambao umejijengea msingi imara ndani na nje ya Tanzania. Ameeleza kuwa muziki huo umefikia hatua ya kuwa sehemu ya utambulisho wa kitamaduni na kiuchumi, hivyo hauwezi kuyumbishwa kirahisi na hisia za muda mfupi.
Kauli yake inakuja wakati ambao baadhi ya Watanzania wanaendelea na wimbi la kususia muziki wa Bongo Fleva, wakieleza kutoridhishwa na hatua za baadhi ya wasanii kujihusisha na siasa wakati wa uchaguzi wa Oktoba uliokumbwa na utata.
Hasira hizo ziliongezeka baada ya kauli ya msanii Diamond Platnumz, aliyewataka vijana kuacha kulalamika na badala yake kufanya kazi, kauli ambayo ilizua mjadala mpana mitandaoni.